VIEWED 1276 TIMES
Young Africans imeendeleza wimbi la ushindi na kuvunjwa mwiko katika michezo ya Ligi Kuu ya Vodacom nchini baada ya kuichpaa timu ya Kagera Sugar mabao 2-1 mchezo uliofanyika dimba la Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.
Kikosi cha Young Africans leo kiliingia uwanjani kwa lengo la kusaka ushindi kwani ilikuwa na kumbukumbu ya kupoteza michezo miwili mfululizo ya Ligi Kuu katika uwanja huu wa Kaitaba.
Mrisho Ngassa alikuwa wa kwanz kuipatia timu yake ya Yanga bao la kwanza dakika ya pili ya mchezo kwa kichwa akimalizia mpira uliorushwa na Mbuyu Twite na kuwapita walinzi na mlinda mlango wa Kagera Sugar na kumkuta mfungaji aliyeukwamisha wavuni bila ajizi.
Yanga iliendelea kulishambulia lango la Kagera Sugar kupitia kwa washambuliaji wake Didider Kavumbagu, Mrisho Ngassa na Hamis Kiiza na dakika ya 25 nusura Niyonzima aipatie Yanga bao lakini shuti lake liliokoloewa na mlinda mlango Aganthony Antony na kuwa kona ambayo haikuzaa matunda.
Mpaka dakika 45 za kipindi cha kwanza zinamalizika, wenyeji Kagera Sugar 0 - 2 Young Africans.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na dakika ya 47 ya mchezo kiungo Boniface Wambura aliipatia Kagera Sugar bao la kusawazisha baada ya mpira uliopigwa na Themi Felix kuokolewa na walinzi wa Yanga na kumkuta mfungaji.
Mara baada ya bao hilo Yanga iliendelea kulishambulia lango la Kagera Sugar kusaka bao la pili na ushindi huku waamuzi wakishindwa kutoa maamuzi mazuri kwani mipira yote kipindi cha pili washambuliaji wa Yanga walionekana wameotea hata kama ni katikati ya uwanja.
Dakika ya 57 Hamis Kiiza aliipatia Young Africans bao la pili na la ushindi baada ya mpira uliopigwa na Mbuyu Twite kuwapita walinzi wa Kagera na kumkuta Kiiza aliyewazidi wepesi na kuachia shuti kali lililotinga moja kwa moja wavuni.
Yanga iliendelea kusaka bao la tatu lakini walinzi wa Kagera Sugar waliokoa mipira ya hatari na kufanya ubao wa matokeo uendelee kusomeka hivyo hivyo.
Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika, wenyeji Kagera Sugar 1 - 2 Young Africans
Kikosi cha Young Africans mara baada ya mchezo wa leo, kesho kitaondoka mjinii Bukoba kurejea jijini Dar es salaam tayari kwa kuanza maandalizi ya mchezo unaofuata dhidi ya Simba SC tarehe 20-10.2013 uwanja wa Taifa.
Young Africans: 1.Barthez, 2.Twite, 3.Luhende, 4.Cannavaro, 5.Yondani, 6.Chuji, 7.Niyonzima/Msuva, 8.Domayo, 9.Kavumbagu, 10.Ngassa, 11.Kiiza/Javu


















