VIEWED 813 TIMES

Young Africans kesho itashuka dimba la uwanja wa Taifa kucheza mchezo wa kirafiki wa kimataifa na timu ya Sports Club Villa kutoka nchini Uganda, mchezo utakaoanza majira ya saa 10:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.
Kikosi cha Young Africans kitautumia mchezo huo wa kirafiki wa kimataifa kwa ajili ya kujiaanda na msimu mpya wa Ligi Kuu nchini na pia itakua ni sehemu ya maandalizi mchezo wa ngao ya Hisani dhidi ya Azam FC jumamosi Agosti 17,2013.
Kocha mkuu wa Yanga Ernie Brandts mara baada ya mazoezi ya leo amesema anashukuru kikosi chake chote kimekamilika na kwa sasa hakuna mchezaji hata mmoja majeruhi hali inayompa nafasi nzuri ya kumtumia mchezaji yoyote katika michezo watakayocheza.
'Mchezo wa kesho dhidi ya Sports Club Villa ya nchini Uganda utakua ni kipimo kizuri kwetu kesho, kwani utakua ni mchezo wa mwisho kabla ya kuanza kwa mikikimikiki ya Ligi Kuu ya Vodacom na kucheza mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Azam FC' alisema Brandts.
Viingilio vya mchezo huo dhidi ya SC Villa ni:
VIP A Tshs 20,000/=
VIP B Tshs 15,000/=
VIP C Tshs 10,000/=
Orange, Blue & Green Tshs 5,000/=
Wapenzi wa soka na washabiki wa klabu ya Yanga wanaombwa kujitokeza kwa wingi kesho kuja kuiona timu ya Yanga ambayo imekamilika kuelekea kwenye kinyang'anyiro cha kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2013/2014



















