VIEWED 1026 TIMES

Mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara msimu wa 2012/2013 timu ya Young Africans leo wameendelea na mazoezi asubuhi katika uwanja wa shule ya sekondari ya Loyola kujiandaa na mchezo dhidi ya timu ya Coastal Union kutoka jijini Tanga mchezo utakaofanyika siku ya jumatano (mei mosi) katika dimba la uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Young Africans ambayo imetawazwa kuwa mabingwa wapya baada ya kufikisha pointi 56 ambazo haziwezi kufikiwa na timu yoyote, imeendelea kujifua chini ya kocha wake mkuu mholanzi Ernie Brandts wachezaji wote wakifanya mazoezi huku wakiwa na morali ya hali ya juu.
Mara baada ya mazoezi kocha mkuu wa Yanga mholanzi Ernie Brandts amesema pamoja na kuwa tayari wameshatangazwa mabingwa wapya, bado kikosi chake kitashuka dimbani kuhakikisha kinaendeleza wimbi la ushindi wa kusaka pointi tatu katika michezo iliyosalia.
"Wengi wanaona kwa kuwa tumeshatwaa ubingwa basi tutapunguza kasi ya ushindi, hilo kwetu hakuna tunaendelea na mazoezi kujiandaa kuhakikisha tunashinda michezo yote iliyosalia na kumaliza ligi kwa rekodi nzuri kuliko timu zote" alisema Brandts.
Katika mchezo wa awali uliofanyika mwishoni mwa mwaka jijini Tanga, Young Africans iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Coastal Union mabao yaliyofungwa na washambuliaji Hamis Kiiza na Didier Kavumbagu
Huu ni Ubingwa wa 24 kwa Yanga tangu kuanzishwa kwa Ligi Kuu Tanzania bara rekodi ambayo hakuna timu yoyote inayokaribia kufuatia watani wa jadi Simba SC kuwa wametwaa ubingwa huo mara 18 tu.
Rekodi ya Ubingwa wa Yanga :1968, 1969, 1970, 1971, 1972, 1974, 1981, 1983, 1985, 1987, 1989, 1991, 1992,1993, 1996, 1997, 1998, 2002, 2005, 2006, 2007-2008, 2008-2009, 2010-2011, 2012-2013
Yanga imebakisha michezo miwili (Costal Union 01.05.2013) na (Simba SC 18.05.2013) kabla ya kumalizika kwa Ligi Kuu ya Vodaom huku ikiwa tayari imeshatwaa Ubingwa mapema kabla ya kumalizika kwa Ligi Kuu ya Vodacom.
Uongozi wa klabu ya Yanga unawaomba wanachama, wapenzi na washabiki wa timu ya Yanga kujitokeza kwa wingi siku ya jumatano (mei mosi) katika dimba la uwanja wa Taifa ili kuja kuwashangilia vijana wakiendeleza furaha ya kutwaa Ubingwa wa VPL msimu huu.
DAIMA MBELE, NYUMA MWIKO (DMNM)
EVER FORWARD, BACKWARD NEVER (EFBN)


















