VIEWED 697 TIMES

Uongozi wa klabu ya Yanga leo umewakabidhi cheti watoto wa marehemu Kilambo Athumani kwa kuutammbua mchango wake ambao aliutoa kwa klabu ya Yanga akiwa kama mchezaji kwa kipindi cha miaka 11 na kuwa kocha mkuu wa klabu Yanga miaka ya 70's.
Kilambo Athuman ambaye alifariki dunia mwezi uliopita na mazishi yake kufanyika katika makaburi ya Kisutu ambapo viongozi mbalimbali wakiongozwa na rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania mh Jakaya Kikwete na mwenyekiti wa klabu ya Yanga Yusuf Mnaji walihudhuria.
Katika enzi za uhai wake marehemu Kilambo aliitumikia klabu ya Yanga kama mchezaji kwa muda wa miaka 11 mfululizo kisha baadae kuitumikia tena klabu ya Yanga kama kocha mkuu.
Akiongea na wandishi wa habari leo makao makuu ya klabu Katibu Mkuu wa Young Africans Lawrence Mwalusako alisema uongozi wa klabu ya Yanga umeamua kufanya hivyo ikiwa ni heshima kwa marehemu Kilambo ambaye alitoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya klabu ya Yanga na Taifa kwa ujumla.
"Uongozi mpya wa Yanga umeona tuwe na utaratibu wa kuwakumbuka wachezaji mbali mbali walioitumikia klabu ya Yanga kwa nyakati tofauti, lengo ni kuwakumbuka wakiwa bado hai kuna utataratibu unafanyika ili kuweza kujua walipo wachezaji wa zamani na kuwa na taarifa zao mara kwa mara" alisema Mwalusako
Akitoa shukrani kwa niaba ya familia ya marehemu mtoto wa kwanza Athumani Kilambo alisema anaushukuru uongozi wa klabu ya Yanga kwa kuwapatia cheti cha heshima, kuutambua mchango wa marehemu baba yao ambaye aliitumikia Yanga kwa kipindi kirefu., hatuna mengi ila tunamuomba mwenyezi mungu ailaze roho ya marehemu mahala pema peponi. Amen.




















