VIEWED 922 TIMES

Baada ya kuwa na mapumziko ya siku mbili kufuatia ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya JKT Ruvu, kikosi cha timu Young Africans Sports Club leo kimeanza tena mazoezi katika uwanja wa shule ya sekondari Loyola kujiandaa na mchezo unaofuata dhidi ya timu ya Coastal Unioni kutoka mkoani Tanga mchezo utakaofanyika jumatao ijayo (Mei Mosi) katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Young Africans ambayo inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom kwa kuwa na pointi 56 ikihitaji pointi 1 tu katika michezo miwili iliyosalia kuweza kutawazwa mabingwa wapya wa VPL 2012/2013 na kufikia mara ya 24 tangu kuanza kwa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Tangu kuanza mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Vodacom Yanga imecheza jumla ya michezo 11 ikiwa imeshinda michezo 8 na kutoka sare michezo 3, imefunga mabao 19 na kufungwa mabao 3 tu katika michezo yote 11 mpaka sasa.
Kocha mkuu Brandts ambaye mwishoni mwa wiki alishindwa kuhudhuria mchezo dhidi ya timu ya JKT Ruvu kutokana na kuumwa malaria, leo ameweza kuongoza mazoezi ya asubuhi baada ya kupona na kurudu katika hali yake ya kawaida.
Akiongea mazoezini amesema anashukuru wachezaji wake na benchi la ufundi kwa kupata ushindi katika mchezo uliopita, ushindi ule dhidi ya JKT Ruvu umeendelea kuongeza nguvu na morali kwetu na kuhakikisha tunashinda michezo mingine iliyosalia kama tuliyojipangia hapo awali.
"Tulisema tangu mwanzo kwamba kila mchezo kwetu ni fainali, na kweli tumekua tukipambana kuhakikisha tunapata ushindi katika kila mchezo, mzunguko wa pili umekua na michezo migumu kwa kila timu kuhitaji pointi lakini tunashukuru tumeweza kupata pointi 27 kati ya 33" alisema Brandts.
Katika mazoezi yaliyofanyika leo uwanja wa shule ya sekondari Loyola wachezaji wote wameweza kufanya mazoezi isipokua mchezaji mmoja tu Juma Abdul ambaye anamalizia matiabu ya kifundo cha mguu alichoumia katika mchezo dhidi ya JKT Oljoro.



















