VIEWED 1615 TIMES

Young Africans leo imeendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom baada ya kuwachapa maafande wa jeshi la kujenga Taifa (JKT Ruvu) kwa mabao 3-0 katika mchezo uliofanyika jioni katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam na kufikisha pointi 56.
Watoto wa Jangwani ambao kwa sasa wanahitaji pointi 1 tu kuweza kutangazwa mabingwa wapya wa Ligi Kuu ya Vodacom, walicheza soka safi na la kuvutia muda wote wa mchezo hali iliyofanya washabiki, wapenzi na wanachama wa Yanga kuwashangilia tangu mwanzo wa mchezo mpaka mwisho.
Yanga iliuanza mchezo kwa kasi kupitia kwa washambuliaji wake Nizar Khalfani, Hamis Kiiza na Saimon ambao walikuwa mwiba mchungu kwa safu ya ulinzi wa timu ya JKT Ruvu ambayo kwa hakika leo ilipata taabu sana.
Saimon Msuva alikosa bao la wazi dakika ya 21 ya mchezo baada ya shuti alilopiga kugongwa mwamba na kutoka nje na kupigwa kona ambayo haikuzaa matunda, huku Nizar Khalfani pia akikosa bao la wazi dakika ya 33 ya mchezo.
Dakika ya 45 kiungo Saimon Msuva aliipatia young Africans bao la kwanza kufuatia mpira uliorushwa kuwazidi walinzi wa JKT Ruvu na kuachia shuti kali liliomshinda mlinda mlango wa JKT Ruvu Shaban Dihile akichumpa bila mafanikio.
Mpaka mpira unakwenda mapumziko, JKT Ruvu 0 - 1 Young Africans.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na Yanga kusaka mbao mengine ya haraka haraka huku wachezaji wake viungo Haruna Niyonzia, Frank Domayo na Athumani Idd 'Chuji' wakitawala sehemu ya kuingo na kugongeana migongeo iliyowachanga viungo wa JKT Ruvu wasijue cha kufanya.
Hamis Kiiza aliipatai Young Africans bao la pili dakika ya 59 kufuatia mpira wa adhabu uliopigwa na David Luhende kumkuta Kiiza ambaye aliwazidi ujanja walinzi wa JKT Ruvu na kuukwamishwa wavuni kwa kichwa na kuhesabu bao la pili kwa watoto wa Jangwani.
Dakika 6 baadae dakika ya 65 mshambuliaji Nizar Khalfani aliipatia Yanga bao la tatu na la ushindi kufuatia kumalizia mpira uliopigwa na Frank Domayo kugonga mwamba na kumkuta Nizar Khalfani aliyeukwamisha wavuni na kuhesabu bao la tatu.
Yanga iliendelea kulishambulia lango la JKT Ruvu muda wote wa mchezo lakini mlinda mlango wao Shaban Dihile alifanya kazi ya ziada kuokoa michomo ya washambuliaji wa timu ya Young Africans.
Mpaka dakika 90 za mchezo zinamalizika, JKT Ruvu 0 - 3 Young Africans.
Kwa matokeo ya leo Young Africans imefikisha jumla ya pointi 56 na mabao 44 ya kufunga na mabao 13 ya kufungwa huku ikiwa imebakiwa na michezo miwili kabla ya kumalizika kwa Ligi Kuu ya Vodacom 2012/2013 pia ikihitaji pointi 1 tu kuweza kutawazwa mabingwa wapya msimu huu.
Yanga itacheza na Coastal Union tarehe 01.05.2013 katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es salam.
Mara baada ya mchezo kocha msaidizi wa Young Africans Fred Felix 'Minziro' alisema anashukuru vijana wake wamecheza vizuri, wamepata nafasi wamezitumia ndio maana tumepata ushindi, Yanga ni timu bora na ili kudhhirisha ubora wake ilibidi tushinde mchezo wa leo ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kutwaa Ubingwa kabla ya kumalziika kwa msimu.
Young Africans: 1.Ally Mustafa 'Barthez'/Said Mohamed, 2.Mbuyu Twite, 3.David Luhende, 4.Nadir Haroub 'Cannavaro', 5.Kelvin Yondani, 6.Athuman Idd 'Chuji', 7.Saimon Msuva, 8.Frank Domayo, 9.Hamis Kiiiza/Jerson Tegete, 10.Nizar Khalfani/Said Bahanuzi, 11.Haruna Niyonzima



















