VIEWED 700 TIMES

Kikosi cha timu ya vijana wenye umri chini ya miaka 20, U-20 cha Young Africans leo kimekata tiketi ya kucheza Robo Fainal ya mashindano ya El Talento Soccer Tournament Cup 2012 baada ya kuichapa timu ya Ayossa FC mabao 5 - 0 katika mchezo uliofanyika katika Uwanja wa Etihad Stadium - Mwananyamala B.
Vijana wa U-20 wa Young Africans wanashiriki mashindano hayo ambayo mshindi ataibuka na zawadi ya tshs Milioni 3, leo walikuwa wanacheza mchezo wa tatu, kufuatia kushinda 2-1 mchezo wake wa kwanza dhidi ya timu ya Mbagala Market, na sare ya 1-1 dhidi ya Star Rangers
Ayossa FC timu ambayo imemaliza hatua ya makundi pasipo kupata pointi hata moja baada ya kufungwa michezo yote, leo walionekana kukakamia mchezo huo, ukizingatia timu ya U-20 Yanga tangu mwezi wa saba (julai) imeshacheza jumla ya michezo 23, ikishinda michezo 18, sare 4 na kufungwa mchezo mmoja tu dhidi ya timu ya Ruvu Shooting katika mchezo wa utangulizi wa ligi kuu ya Vodacom.
U-20 Yanga waliuanza chezo kwa kasi kwa lengo la kusaka bao la mapema, katika dakika ya 16 kiungo mshambuliaji Rehani Kibingu aliipatia timu ya U-20 bao la kwanza akimalizia kazi nzuri ya George Banda.
Dakika ya 32, Rehani Kibingu tena aliipatia U-20 bao la pili baada ya kuwazidi ujanja walinzi wa Ayossa na kuachia shuti kali lililojaa wavuni moja kwa moja.
Mpira ulikwenda mapumziko, U-20 Yanga 2- 0 Ayossa FC
Kipindi cha pili kilianza kwa kocha mkuu wa U-20 Young Africans kufanya mabadiliko, ya kuwaingiza Notikelly Masasi, Hussein Moshi kuchukua nafasi za Suleiman Ussi na Clever Charles.
Mabdiliko hayo yalileta uhai kwa kikosi cha U-20 kwani dakika ya 46 ya mchezo, mshambuliaji Notikely Masasi aliipatia U-20 bao la tatu kwa njia ya tik tak, akiunganisha krosi safi ya Zuberi Amiri.
Notikely Masasi aliendelea kuwa mwiba kwa walinzi wa Ayossa kwani katika dakika ya 72 ya mchezo aliipatia U-20 bao la nne akimalizia krosi ya Mwinyi Bakari aliywatoka walinzi wa Ayossa na kupiga krosi iliyomkuta mfungaji.
Dakika ya 85, Zuberi Amiri aliipatia U-20 Yanga bao la tano baada ya kupanda kusaidia mashambulizi na kumtoka mlinzi wa Ayossa kisha kumpiga chenga mlinda mlango kabla ya kufunga bao hilo.
Mpaka dakika 90 zinamalizika, U-20 Young Africans 5 - 0 Ayossa FC.
Kwa matokeo hayo U-20 Young Africans imeongeza kundi D kwa kufikisha point 7 baada ya kushinda michezo miwili na kutoka sare mchezo mmoja, hivyo itacheza mchezo wa Robo Fainali siku ya jumatatu saa 1 kasorobo usiku dhidi ya timu ya African People.
Mchezo wa leo ulihudhuriwa na kocha mkuu Ernie Brands aliyekuwa akitazama vipaji vya vijana.
U-20 Yanga: 1.Yusuph Abdallah, 2.Zuberi Amiri, 3.Said Mashaka/Hussein Moshi, 4.Benson Michael, 5.Issa Ngao, 6.Clever Charles 7.Rehani Kibingu, 8.Mwinyi Bakari, 9.George Banda 10.Suleiman Ussi/Notikelly Masasi 11.Abdallah Mnguli














