VIEWED 719 TIMES

Timu ya Young Africans Sports Club yenye makao yake makuu, makutano ya mitaa ya Twiga/Jangwani itacheza na timu ya Azam Fc siku ya jumapili katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania bara mchezo utakaofanyika Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Young Africans ambayo mpaka sasa imejikusanyia jumla ya pointi 23 baada ya kucheza michezo 11, kushinda michezo 7, kutoka sare michezo 2 na kufungwa michezo 2, imefunga jumla ya mabao 21 na kufungwa mabao 10, inakamata nafasi ya pili kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa dhidi ya Simba SC.
Kikosi cha wachezaji 30 na benchi la ufundi 7 wameingia kambini jana jioni katika hoteli ya kitalii ya Kiromo iliyopo eneo la Bagamoyo ambapo leo asubuhi wachezaji wamefanya mazoezi katika uwanja wa mbegani na hakuna majeruhi yoyote.
Kocha mkuu wa Young Africans mholanzi Ernie Brandts amesema kikosi chake kipo vizuri na maandalizi ya mchezo wa jumapili yako safi kabisa, na anaamini timu yake itaibuk ana ushindi katika mchezo huo na kuendelea kujiweka katika nafasi nzuri ya kutwaa Ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom 2012/2013.
Jana nilikwenda Uwanja wa Chamanzi kutazama mchezo kati ya Azam FC na Coastal Union timu ambazo ndio pekee tumebakisha michezo 2 nazo katika kumalizia mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Tanzania bara, utakaomalizika novemba 11, 2012, nimefanikiwa kujua mifumo na mbinu wanazotumia kucheza hivyo naamini tutafanya vizuri alisema 'Brandts'
Mshambuliaji Didier Kavumbagu wa timu ya Young Africans ndie kinara wa mabao mpaka sasa katika Ligi Kuu ya Vodacom, akiwa na jumla ya mabao 6, ataendelea kusaka magoli zaidi ili kuweza kujitengenezea mazingira mazuri ya kuibuka mfungaji bora.














