ARTICLE HITS: 473 TIMES
Wachezaji wa kimataifa kutoka nchini Ghana, Kenneth Asamoah na Yaw Berko wameondoka jijini Dar es Salaam alfajiri ya leo kwenda nchini Ghana kwa ajili ya mapunziko ya muda mfupi. Wachezaji hao wameondoka baada ya Uongozi wa mabingwa wa soka kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati kutoa mapunziko ya wiki tatu kabla ya kuingia katika hatua nyingine ya mzunguko wa ligi kuu pamoja na michuano ya kimataifa inayoikabili Klabu ya Yanga ikiwemo mashindano ya Klabu Bingwa barani Afrika na michuano ya Kombe la Kagame. Akizungumza na www.youngafricans.co.tz , Afisa Habari wa Klabu ya Yanga,
Louis Sendeu amesema kuondoka kwa wachezaji hao ni kwa ajili ya kwenda kuungana na familia zao ambazo kwa kipindi kirefu hawakupata nafasi ya kuwa nao. Sendeu amesema likizo ya wachezaji wote wa Yanga iliyokuwa imeanza tangu tarehe 3 mwezi huu inatarajia kumalizika tarehe 27 mwezi huu ambapo siku itakayofuata wachezaji hao wanatarajia kuanza mazoezi ya kujiandaa na hatua ya pili ya ligi kuu ya Vodacom pamoja na michuano ya kimataifa ambayo inatarajia kuanza mapema Mwakani. Aidha Sendeu amesema mchezaji Davies Mwape ndiye mchezaji pekee aliyebakia ambaye anatarajia kuondoka kesho na shirika la ndege la Kenya -KQ majira ya asubuhi. Akizungumzia Kocha Mkuu Kostadian Papic, Msemaji huyo amesema kocha huyo ataendelea na shughuli za Klabu ikiwemo maandalizi ya Programu pamoja na zoezi la usajiri kupitia dirisha dogo linaloendelea hivi sasa.















